MAMBO YA KUSHANGAZA KUHUSU KIFO.
MAMBO YA KUSHANGAZA KUHUSU KIFO.
Kifo limekuwa jambo lenye kuogopwa na wengi kiasi kwamba siku hizi imekuwa nadra sana kuzungumziwa na watu, lengo lao likiwa ni kujifariji na kujisahaulisha kuwa siku moja watakufa. Hali hii imepewa jina kitaalamu inaitwa 'Thanatophobia' neno lenye maana "hofu ya kifo." Watalamu wa mambo ya saikolojia wamebainisha kuwa kwa kawaida kimtishacho binadamu ni kile asichokijua (Fear of the unknown), hali hii pia inaitwa Xenophobia. Hivyo wengi hukiogopa kifo kwa sababu hawakijui. Kuufahamu ukweli kuhusu kifo kutakusaidia kuendelea kuwa jasiri na kukuondolea hofu iliyojengeka ndani yetu kuhusu hatma ya kila mmoja wetu.
KIFO NI NINI?
Kuna nadharia nyingi sana kuhusu kifo. Nyingi kati ya nadharia hizo zimejikita zaidi katika masuala ya kidini na kiimani. Taarifa tulizonazo kisayansi kuhusu kifo ni kidogo sana hivi kwamba maswali yaliyopo ni mengi kuliko majibu. Kitabu Reasoning From The Scriptures kinaeleza kuwa kifo, "ni kukoma kwa utendaji wote wa uhai. Baada ya mtu kuacha kupumua, moyo wake kuacha kupiga, na ubongo wake kuacha kutenda, hatua kwa hatua nguvu za uhai huacha kutenda kazi katika chembe za mwili wake." Lakini kutokana na maendeleo ya kitabibu mtu aliyekufa anaweza kurudishwa tena katika uhai, kwani imethibitika kuwa mtu anapokufa chembe zilizo ndani ya mwili wake huendelea kufanya kazi kwa masaa kadhaa kabla mwili haujaanza kuharibika. Ndani ya muda huo kwa kutumia mbinu za kisasa zilizoboreshwa kuna uwezekano wa kumrudisha mfu huyo kwenye uzima. Ripoti kadhaa za kitabibu zimethibitisha kuwa mtu anapokata roho yaani mapigo ya moyo wake na upumuaji vinaposimama, katika hali isiyo ya kawaida mtu huyo huwa na uwezo wa kusikia, kuhisi na kutambua shughuli mbalimbali zinazoendelea kando yake dakika kadhaa za mwanzo anapofariki kisha uwezo huo huendelea kufifia hatua kwa hatua hadi unapokoma kabisa.
KUKIKARIBIA KIFO
Near Death Experience (NDEs) ni hali ambayo baadhi ya watu wamewahi kupitia pengine baada ya kuugua sana hivi kwamba ikadhaniwa wamekufa baada ya pumzi na mapigo yao ya moyo kusimama. Baada ya mtu kuacha kupumua na moyo kuacha kupiga, inachukua dakika kadhaa kabla ya nguvu za uhai kukoma hatua kwa hatua katika chembe zake mwilini. Jambo hilo linaweza kukawizwa kwa saa kadhaa mwili unapowekwa kwenye baridi kali. Kwa sababu hiyo, mara nyingine inawezekana kumrudishia mtu fahamu kwa kuanzisha tena utendaji wa moyo na mapafu. Ingawa alionwa kana kwamba amekufa, chembe zake za mwili zilikuwa bado zingali hai. Watu wengi waliorudiwa na fahamu baada ya "kifo" cha aina hiyo, hawakumbuki lolote. Wengine husimulia kuwa walihisi ni kana kwamba walikuwa wakielea. Wengine husema waliona vitu vizuri n.k.
SHUHUDA ZA WATU WALIOWAHI KUKIKARIBIA KIFO.
Kuna baadhi ya matukio tofauti tofauti ambayo husimuliwa na watu hawa ambao wamewahi kupitia hali hii ya Near Death Experiences (NDEs). Japo kila mtu husimulia alichokiona kwa namna yake lakini kuna ufanano mkubwa wa matukio kadhaa baina ya simulizi za watu hao. Baadhi ya matukio yaliyo simuliwa na watu hao yenye kufanana sana ni kama; walipokuwa katika hali hiyo ya kifo walijikuta wakiwa katika miili mipya isiyo na kasoro wakiwa wenye amani na utulivu. Au mara nyingine walijikuta wakiwa katika eneo lililozungukwa na mwanga mkali pande zote wakiitazama dunia kwa mapana yake na wasione chochote kulia wala kushoto isipokuwa mwanga mkali. Kati ya simulizi hizo nyingi kuna ushuhuda maarufu uliowahi kutolewa na mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Pam Reynold. Mama huyu alipatwa na ugonjwa uitwao Basilar Artery Aneurysm unaosababishwa na kupasuka kwa mshipa ulio nyuma ya ubongo (Basilar Artery). Ushuhuda huu upo kwenye kitabu cha daktari aliyekuwa akimfanyia utafiti mwanamke huyu, Dr. Michael Sabom, kiitwacho Light and death.
Dr. Michael baada ya kugundua tatizo la Bi. Pam, alimrufaa kwa daktari aliyekuwa mtaalam wa upasuaji wa ubongo wa ugonjwa huu, upasuaji ambao ni hatari na hufanyika mara chache sana. Upasuaji huo unafahamika kwa jina la Hypothermic Cardiac Arrest lakini ulipewa jina la utani la "Standstill". Ili upasuaji huu ufanyike inatakiwa mgonjwa afanyiwe taratibu zifuatazo (Procedures):
1. Jotoridi la mwili lazima lishushwe hadi kufikia nyuzi 16 °C kutoka nyuzi 37 °C za joto la kawaida,
2. Mapigo ya moyo na kupumua kuzuiliwe,
3. Damu iondolewe kwenye kichwa na
4. Ubongo usifanye kazi.
Kwa kifupi ni kufa ndani ya muda fulani!
Kwa mujibu wa Bi. Pam baada ya kufanyiwa mambo haya kwenye upasuaji wake, ulifika wakati akajiona anatoka katika mwili wake halisi na kukaa pembeni. Aliona jinsi madaktari walivyokuwa wakiufanyia mwili wake upasuaji. Akiwa pembeni alizisikia sauti zikimwita "Njoo" lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida. Alianza kusogea huku akiwa ameuacha mwili wake pale kitandani ukifanyiwa upasuaji akielekea kulikokuwa na zile sauti ambazo alianza kuzitambua, mojawapo ikiwa ni sauti ya bibi yake aliyefariki kipindi cha nyuma. Sauti hizo ambazo zilikuwa zikitoka kwenye mwanga mkali alipozifikia ndipo aliweza kuwaona ndugu zake mbalimbali ambao walishafariki. Bi Pam alitaka kuingia katikati ya ule mwanga mkali lakini baba yake mdogo ambaye naye alikuwa miongoni mwa wale watu aliowaona alimzuia akimwambia kuwa endapo akiingia katika mwanga huo hawatakuwa na uwezo wa kumrudisha kwenye mwili wake.
Baba yake mdogo ndiye aliyemchukua na kumrudisha pale ulipokuwa mwili wake. Kwa mujibu wa Bi. Pam anasema hakutaka kurudi kwenye mwili wake ule wa mwanzo kwa jinsi alivyokuwa akijisikia amani katika ulimwengu huo mpya.
UNACHOPASWA KUKIFAHAMU KUHUSU NEAR DEATH EXPERIENCES (NDEs)
Nilikutana na simulizi la mama huyu nilipokuwa nikitafuta taarifa na vithibitisho rejea vya ushahidi ili kuleta makala yenye mtiririko unaoeleweka. Changamoto niliyokutana nayo katika Ushuhuda wa mama huyu ni kuhusu utata uliopo kwenye simulizi za namna hii. Pamoja na kwamba simulizi hili hata lilirekodiwa na kuandikwa kwenye kitabu cha daktari aliyekuwa akimfanyia utafiti, Dr. Michael Sabom. Shuhuda hizi zimetokea kugubikwa na utata mkubwa mno hasa baada ya kuchapishwa kwa matokeo ya uchunguzi uliofanyika kuhusu uhalali wa habari zinazotolewa na watu ambao wamerudiwa na fahamu baada ya kusemekana kwamba walikufa. Jarida la tiba la Ujerumani Fortschritte Der Mezidin, linafafanua kuwa wakati nguvu za mwili zinapopungua sana, mathalani wakati mtu anapopewa dawa ya kuondoa fahamu, au kwa sababu ya magonjwa au majeraha, uwezo wa mwili wa kuendeleza utendaji mbalimbali mwilini hupungua sana. Kwa hiyo, homoni za neva na umajimaji mwingine wa mfumo wa neva huenea kwa wingi mwilini. Matokeo yake ni kwamba mtu huyo anaweza kuona na kusikia mambo yasiyokuwako ambayo baada ya kurudiwa na fahamu humfanya afikiri kwamba alikuwa ameona yaliyo kwenye ulimwengu mwingine na sasa amefufuka.
MSIMAMO WA DINI KUHUSU KIFO.
Karibia waumini wa dini zote kubwa ulimwenguni wanaungana kuamini kuwa binadamu alipata kuwepo duniani kutokana na Mungu. Wasomi wengi hukadiria kuwa kuna zaidi ya dini 4,200 ulimwenguni. Karibu watu billion 6 hutoka katika imani fulani ya kidini, isitoshe zaidi ya 57% ya idadi ya watu wote ni eidha wakristo ama waislamu. Hii inamaanisha dini hizi mbili zimeenea kwa kiwango kikubwa ulimwenguni na kujipatia waumini wengi kuliko dini nyingine zote! Katika tafiti yetu tutaangazia dini hizo mbili kuu, yaani ukristo na uislamu. Tutagusia kwa uchache maoni ya dini hizo kuhusu kifo, tukianza na uislamu. Uislamu unasema nini kuhusu kifo?
UISLAMU UNASEMA NINI KUHUSU KIFO?
Uislamu unasema kwamba binadamu ana nafsi isiyoweza kufa, hii inamaanisha mtu anapokufa huendelea kuwa na utambuzi wake timilifu akifahamu kila kinachoendelea wakati huo ijapokuwa yu mfu tayari. Utambuzi huo haukomi hata anapotiwa kaburini. Maisha kuanzia mtu anapokufa huitwa ‘Maisha Ya Barzakh’. Barzakh au 'kiambaza' hurejelewa kama kipindi baina ya wakati wa mauti na Qiyaamah. Waislamu huamini kuwa maisha ya Barzakh yanayotofautiana kabisa na maisha ya duniani, na hakuna ajuaye hakika kamili ya maisha haya na namna yalivyo isipokuwa Allaah pekee. Inaaminika kuwa kila maiti atapitia katika maisha hayo, awe Muislam au kafiri, mwema au mwovu, na katika kipindi hicho kunakuwa na fitna ya kaburi ambako mtu anajiwa na Malaika wawili kuhojiwa na kisha hufuatia neema au adhabu za kaburini.
Maisha ya kaburini au Barzakh hufafanuliwa kuwa kipindi anachokaa mtu baada ya kufa kwake mpaka kufufuliwa kwake. Kipindi kati ya parapanda la kwanza ambalo ni amri ya kufa viumbe vyote na parapanda la pili ambalo ni amri ya kufufuliwa viumbe vyote vitakavyotakiwa vifufuke. Tunajulishwa kuhusu Barzakh katika Aayah ifuatayo:
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾
Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: Rabb wangu! Nirejeshe (duniani). Ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha. (Ataambiwa) Laa hasha! Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu. Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa. [Al-Muuminuwn: 99-100].
Katika kipindi hiki cha maisha mapya ni mambo gani yanayoendelea katika nafsi ya mwenye kufa?
Inaaminika katika kipindi hiki cha Barzakh roho za watu wema zitakaa pahali pazuri kungojea malipo yao ya Peponi, Ama zile za watu waovu zitakuwa mahabusu zikingojea siku ya hukumu yao. Hivi ndivyo tunavyojulishwa katika Hadiyth zifuatazo:
(Hadiyth ni simulizi zilizo andikwa na watu kuhusu matendo, walivyomuona au walivyomsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam/S.A.W.)
Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesimulia kutoka kwa Mtume/Rasuli wa Allaah (S.A.W.) ambae alisema:
“Hakika maiti hupelekwa kaburini na hukaa kaburini bila ya khofu wala fadhaa. Baada ya hapo ataambiwa: “Ulikuwa katika nini? Atajibu: “Muhammad Rasuli wa Allaah (S.A.W) alitujia na hoja zilizokuwa wazi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) na kwa hivyo tulimuamini. Ataulizwa tena “Umemuona Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa)? Atajibu: “Si katika uwezo wa yeyote kumuona Allaah (‘Azza Wa Jalla). Kisha patawekwa uwazi utakaomuonyesha moto unaofoka. Kisha ataambiwa angalia kile ambacho Allaah Amekuokoa (Amekukinga nacho). Kisha patawekwa uwazi utakaomuwezesha kuiona Jannah (Pepo) na pia vyote vilivyomo ndani yake. Ataambiwa: “Hii ni sehemu yako kutokana na Uthibiti wa Iymaan uliyoishi nayo hadi kufa nayo na ambayo utafufuliwa nayo In Shaa Allaah”.
Ama kuhusu mtu muovu yeye atakaa katika kaburi lake kwa khofu na fadhaa. Ataulizwa: Ulikuwa katika nini? Atajibu sijui. Kisha ataulizwa tena: Ni nani huyu? Atajibu nilisikia watu wakisema kama nilivyosema. Kisha utawekwa uwazi kwa kumuwezesha kuiona Jannah ataangalia na kuona uzuri wake na vilivyomo ndani yake. Ataambiwa: Angalia kile ambacho Allaah (Subhaanahu Wa Ta’aalaa) Amekukosesha (Kutokana na Iymaan yako mbovu). Kisha utawekwa Moto uwazi wa kumuwezesha kuona na ataambiwa hii ndio sehemu yako ambayo uliendesha maisha yako kwa kuwa na mashaka nayo, na umekufa ukiwa na mashaka nayo na utafufuliwa ukiwa katika hali hiyo hiyo, In Shaa Allaah”.
Pia tukiangalia katika Hadiyth nyingine inatueleza kuwa;
“Malaika wawili watamjia (maiti), Watamkalisha na kumuuliza: Ni nani Rabb wako? Atajibu “Allaah pekee Ndiye Rabb wangu.” Kisha watamuuliza tena, Ni nani huyo aliyeletwa kwenu? Atajibu: “Alikuwa ni Rasuli wa Allaah (S.A.W).” Watamuuliza tena; Amekuleteeni habari gani? Atajibu: “Nimesoma kitabu cha Allaah nikaamini kutokana nacho na nikaithibitisha ‘Iymaan hiyo (katika matendo)”.
Na pia tuangalie Kauli Yake Mtume Rasuli wa Allaah (S.A.W) anasema:
“Mtangazaji (mwenye kunadi) atatangaza (atanadi) kutoka mbinguni: Hakika mja Wangu amesema ukweli. Mtengeeni sehemu Jannah (Peponi) na mvisheni mavazi ya Jannah, Na mfungulieni mlango wa Jannah. Kisha utafunguliwa. Akasema Rasuli wa Allaah (S.A.W) na hewa ya Jannah na harufu yake nzuri ya manukato itamjia na Jannah itakurubishwa kwake kiasi cha upeo wa macho yake.
Ama kwa kafiri asiyeamini, Rasuli wa Allaah (S.A.W), alitaja kifo chake akisema: Roho yake itarudishwa katika kiwiliwili chake na Malaika wawili watamjia, Watamkalisha na kumuuliza: Ni nani Rabb wako? Atajibu: Sijui!
Watamuuliza tena: Ni ipi dini yako? Atajibu: Sijui!
Kisha watamuuliza ni nani huyo aliyeletwa kwenu? Atajibu: Sijui!
Kisha mwenye kunadi atanadi kutoka mbinguni: Hakika amesema uongo, Kwa hiyo mkunjulieni kitanda cha motoni. Akasema Rasuli wa Allaah (S.A.W) Kisha joto lake na upepo wa moto utamjia na kaburi lake litakuwa jembamba sana kwake mpaka mbavu zake mbili zitapishana. Kisha atakabidhiwa kwa Malaika kipofu na kiziwi mwenye pande (rungu) la chuma, Kama mlima ungelipigwa na chuma hicho ungelikuwa vumbi. Atampiga kwa chuma hicho kwa kipigo ambacho kitasikika kwa kila aliye Mashariki na Magharibi isipokuwa viumbe wa aina mbili (Majini na Watu) hawatasikia. Atakuwa vumbi na kisha roho itarudishwa tena kwake.”
(Hii ndiyo tamati ya ufafanuzi wa kifo katika Uislamu)
UKRISTO HUSEMA NINI JUU YA KIFO?
Ukristo umegawanyika katika madhehebu mbalimbali, kati ya imani kuu za msingi kwenye madhehebu hayo ni imani juu ya utatu mtakatifu na maisha baada ya kifo ama "roho isiyoweza kufa." Biblia inasema nini kuhusu utatu na kifo? Kabla ya kuwasilisha utata uliopo baina ya mafundisho hayo na maandiko matakatifu ya Biblia, acha kwanza tuanze na ufafanuzi wa mafundisho yenyewe. Hii itatusaidia kuelewa kiundani jinsi hoja zilizojengeka kibliblia juu ya kifo zinavyo hitilafiana kwa kiwango kikubwa na maoni ya wakristo walio wengi. Tukianza na utatu mtakatifu. Wanaoamini katika utatu husema nini?
Kutokana na utata uliopo katika kulifafanua fundisho hilo madhehebu yanayolitumia kwenye imani zao hudokeza kuwa hilo ni "fumbo" lililo kwenye "Dogma ya imani." Dogma hurejelea fundisho la imani lisiloweza kukanushwa na wafuasi wa imani husika. Mwamini anayekataa dogma huhesabiwa kuwa mzushi na hutengwa na Kanisa. Basi, fumbo hilo la utatu hufafanuliwaje na wanaoliamini?
KANISA Katoliki la Kiroma hutaarifu hivi: “Kwa kutumia maneno ya Imani ya Athanasio: ‘Baba ni Mungu, Mwana (Yesu) ni Mungu, na Roho Mtakatifu ni Mungu, na bado hakuna Miungu watatu bali Mungu mmoja.’ Katika Utatu huu . . . Nafsi au Watu hao watatu wana umilele-sawa na cheo-sawa: wote hali yao ni moja hawakuumbwa, hawana mwanzo na wana uweza wote.”—The Catholic Encyclopedia.
JE, MAANDIKO MATAKATIFU YA BIBLIA YANAUNGA MKONO FUNDISHO HILO?
Wengi wanaoamini fundisho la Utatu hukubali kwamba hawawezi kulieleza. Lakini, huenda wakafikiri kwamba hilo ni fundisho la Biblia. Ni muhimu kutambua kwamba neno “Utatu” halipatikani kamwe katika Biblia. Lakini je, wazo lenyewe linapatikana katika Biblia? Ili kujibu swali hilo, hebu tuchunguze andiko ambalo wanaounga mkono fundisho hilo hutumia kutetea Utatu.
“NENO ALIKUWA MUNGU”
Tufuatane kwa umakini hapa!
Andiko la Yohana 1:1 linasema: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.” (Union Version) Baadaye, katika sura hiyohiyo, mtume Yohana anaonyesha waziwazi kwamba “Neno” ni Yesu. (Yohana 1:14) Hata hivyo, kwa kuwa Neno anaitwa Mungu, baadhi ya watu hukata kauli kwamba Mwana (Yesu) na Baba ni Mungu yuleyule.
Kumbuka kwamba mwanzoni sehemu hiyo ya Biblia iliandikwa katika Kigiriki. Baadaye, mstari huo wa Kigiriki ulitafsiriwa katika lugha nyingine. Hata hivyo, watafsiri fulani wa Biblia hawakusema “Neno alikuwa Mungu.” Kwa nini? Kulingana na ufahamu wao wa lugha ya Kigiriki iliyotumiwa kuandika Biblia, watafsiri hao walikata kauli kwamba maneno “Neno alikuwa Mungu” yalipaswa kutafsiriwa tofauti. Jinsi gani? Kuna mifano michache hapa: “Logos [Neno] alikuwa na sifa za kimungu.” (A New Translation of the Bible) “Neno alikuwa pamoja na Mungu na alikuwa na utu kama wake.” (The Translator’s New Testament) Kulingana na tafsiri hizo, Neno si Mungu mwenyewe. Badala yake, kwa sababu ya ukuu wake miongoni mwa viumbe wa Mungu, Neno anaitwa “Mungu” ikirejelewa kuwa alikuwa na sifa au muonekano, utu na tabia kama za Mungu Mweza.
PATA HABARI ZAIDI
Watu wengi hawajui Kigiriki kilichotumiwa kuiandika Biblia. Basi unawezaje kujua alichomaanisha mtume Yohana? ili kuelewa vizuri maana ya Yohana 1:1, unaweza kutafuta habari zaidi kuhusu cheo cha Yesu katika Injili hiyo hiyo ya Yohana ama katika injili zingine. Kupata habari zaidi kutakusaidia kujua ukweli.
Kwa mfano, fikiria yale ambayo Yohana aliandika katika sura ya 1, mstari wa 18: “Hakuna mwanadamu amemwona Mungu [Mweza-Yote] wakati wowote.” Hata hivyo, wanadamu walimwona Yesu.
Yohana anasema pia kwamba Neno alikuwa “pamoja na Mungu.” Basi, mtu anawezaje kuwa pamoja na mtu mwingine na wakati huohuo awe ndiye mtu huyo? Isitoshe, katika Yohana 17:3, Yesu anaonyesha waziwazi tofauti iliyopo kati yake na Baba yake wa mbinguni. Anamwita Baba yake “Mungu wa pekee wa kweli.” Kisha Yohana anasema hivi mwishoni-mwishoni mwa Injili yake: “Haya yameandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo Mwana wa Mungu.” (Yohana 20:31) Ona kwamba Yesu anaitwa, Mwana wa Mungu, wala haitwi Mungu. Habari hiyo ya ziada iliyo katika Injili ya Yohana inatusaidia kuelewa andiko la Yohana 1:1. Yesu, yule Neno, ni “mungu” katika maana ya kwamba ana cheo cha juu lakini siye Mungu Mweza-Yote.
CHANGANUA UTHIBITISHO
Hebu fikiria pia aliyoandika Mathayo kuhusu mwisho wa ulimwengu huu, anamnukuu Yesu akisema: “Kuhusu siku ile na saa ile hakuna mtu anayejua, wala malaika wa mbinguni wala Mwana, ila Baba tu.” (Mathayo 24:36) Maneno hayo yanathibitishaje kwamba Yesu si Mungu Mweza-Yote?
Yesu mwenyewe anasema kwamba Baba anajua mambo mengi kuliko Mwana. Hata hivyo, ikiwa Yesu angekuwa ndiye Mungu Mweza-Yote, angejua mambo yote anayojua Baba yake. Kwa hiyo, basi, Mwana na Baba hawalingani. Suala hilo limerudiwa pia kwenye andiko la Yohana 14:28. Katika andiko hili Yesu alisema "Baba ni mkuu kuliko mimi."
JE, YESU HANA MWANZO KAMA ALIVYO BABA YAKE?
Wakolosai sura ya 1 aya ya 15 hubainisha kuwa;
"Yeye [Yesu] ndiye mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote." Andiko hili linatusaidia kuelewa kuwa kumbe Yesu ndiye alikuwa mwanzo wa uumbaji wote wa Mwenyezi Mungu.
YESU KRISTO NI KIUNGO MUHIMU MNO BAINA YETU NA MUNGU, JINSI GANI?
Maandiko matakatifu yanasema;
“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maana..... Yeyote amwaminiye [Yesu] hahukumiwi, lakini asiyeamini amekwisha kuhukumiwa, kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Yohana 3:16-18.
Katika kutilia mkazo daraka hilo Yesu alisema;
“Mimi ndimi njia na kweli na uzima. Mtu hawezi kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia kwangu. YOHANA 14:6
Hii inamaanisha kupitia dhabihu ya Yesu Kristo sisi sote tunapendeleo la kupata tumaini jipya, tunapokea msamaha wa dhambi zetu na zaidi uzima wa milele!
BAADA YA KUJIFUNZA SOMO HILO MUHIMU, HEBU SASA, TUGEUKIE KUUTAZAMA MSIMAMO WA UKRISTO JUU YA KIFO.
Maandiko matakatifu yanafafanuaje suala hilo. Biblia takatifu inafananisha kifo na hali ya kulala usingizi mzito usio na ndoto. Tunaposoma andiko la Yohana sura ya 11 kuanzia aya ya 11, tunakutana na simulizi la Lazaro rafiki yake Yesu aliyeishi Bethania. Biblia inasema baada ya Lazaro kufa alikaa kaburini kwa muda wa siku nne kabla ya kufufuliwa na Yesu. Katika simulizi hilo, Lazaro alipokufa Yesu aliwaambia wanafunzi wake akisema;
"Rafiki yetu, Lazaro, amelala; lakini ninakwenda nipate kumwamsha."
Akitilia mkazo suala hilo Yesu alisema waziwazi kuwa "Lazaro amekufa."
Yohana 11:11-14.
Hata tunaposoma kitabu cha Zaburi 13:3 maandiko hayo yanakazia wazo lile lile juu ya mfanano uliopo baina ya kifo na usingizi mzito. Zaburi 13:3 inasema "Ee BWANA, Mungu wangu... Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti."
JE, KUNA SEHEMU FULANI YA MTU INAYOENDELEA KUISHI BAADA YA MWILI KUFA?
Karibu dini zote za zamani na za sasa, huamini kwamba sisi huendelea kuishi tukiwa na uwezo wa kuona, kusikia, na kufikiri baada ya mwili kufa. Biblia ina maoni gani kuhusu jambo hilo? katika kitabu cha Mhubiri 9:5-6. Andiko hili linaweka bayana ukweli huu ulio wazi linaposema:
"Walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu HAWAJUI neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua."
Soma pia Isaya. 26:14
"Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki...... "
Maandiko haya yanaweka bayana hali ya wafu kuwa hakuna sehemu yoyote ya mtu inayoendelea kuishi baada ya kifo. Hata hivyo wanasayansi na madaktari wa upasuaji hawajaona uthibitisho wa kuwapo kwa sehemu yoyote ya mwanadamu iliyo na ufahamu na inayoendelea kuishi baada ya mwili kufa.
Natumai kuwa utakuwa umenufaika na kujifunza mambo mengi juu ya ufafanuzi wa mada hii muhimu, kuhusu kifo. Utafiti huu ulifanyika kwa lengo la kuimarisha imani zetu na kubainisha hoja zilizo wazi juu ya maana, maoni ya kisayansi na kidini kuhusu kifo kwa namna ya kujenga. AHSANTE...

Maoni
Chapisha Maoni