UMUHIMU WA AMANI
AMANI
Kamusi elezo ya mtandaoni Wikipedia, inaeleza kwamba "amani ni hali ya raha na usalama bila ugomvi; au kwa maneno mengine amani ni kinyume cha fujo au vita." Ni ndoto ya kila mtu kuishi maisha yenye amani na furaha. Karibia kila kitu tunachokifanya ni kwa sababu tunahitaji amani. Tunatamani mambo yote kutia ndani ndoa zetu zingedumu kwenye amani lakini wapi! Mataifa yanahaha kuisaka amani kwa mtutu wa bunduki. Wenye hekima na vitabu vingi vinavyoheshimika wamethibitisha thamani iliyopo katika amani, mathalani Biblia takatifu kwenye kitabu cha Methali Sura 17 mstari wa kwanza inasema "Ni afadhali kipande kikavu cha mkate mahali penye amani, Kuliko nyumba iliyojaa karamu pamoja na ugomvi."
Historia ya mwanadamu inaonyesha jitihada kubwa ambazo binadamu amezifanya kwa miaka mingi kuitafuta amani, kwa mfano baada ya vita vya kwanza vya ulimwengu vilivyopiganwa 1914 hadi 1918 kuisha, mapema mwaka 1919 mataifa washindi kwenye vita hiyo walianzisha Shirikisho la Mataifa au League of Nations pendekezo lililotolewa na rais wa marekani kipindi hicho Woodrow Wilson. Alipendekeza hatua za kuanzisha shirikisho hili kwa kusudi la kuzuia vita kwa wakati ujao baada ya mwisho wa vita ile ya kwanza. Shirikisho hili kwa njia fulani lilisaidia kusuluhisha baadhi ya misuguano iliyokuwepo baina ya mataifa kadhaa kama mgogoro kati ya Albania na Yugoslavia kuhusu mipaka ya Albania, mashambulio ya ugiriki dhidi ya Bulgaria n.k. Licha ya mafanikio hayo Shirikisho la Mataifa lilishindwa kudumisha amani ya ulimwengu hata kati ya mataifa wanachama mfano China iliposhambuliwa na Japan 1931, Italia ilipovamia Ethiopia ikitumia silaha za gesi zilizopigwa marufuku Shirikisho la Mataifa halikuchuakua hatua yoyote. Hata Ujerumani ilipoongeza jeshi lake kupita kiwango kilichokubaliwa Shirikisho la Mataifa walinyamaza tu. Matokeo yake ilikuwa mapema Septemba 1939 Ujerumani ilipovamia Poland. Baada ya siku chache tu vita kuu ya pili ya ulimwengu ikaanza. Ajabu ni kuwa marekani ambayo ilikuwa mstari wa mbele kuandaa kuundwa kwa Shirikisho la Mataifa ili kulinda amani ya ulimwengu na kuzuia vita, kwa kutumia ndege yao maalumu ya kubeba na kudodosha mabomu aina ya American B-29 Bomber tarehe 6 Agosti ya mwaka 1945 walidondosha bomu hatari la nyuklia katika mji wa Hiroshima ulio nchini Japan. Mlipuko huo uliua watu takribani 80,000 na kuacha wengine zaidi ya 10,000 ambao wangefariki kutokana na athari za mionzi yake. Siku tatu baadaye yaani tarehe 9 Agosti kwa kutumia ndege nyingine ya B-29 Bomber waliachia bomu jingine katika mji wa Nagasaki lililokadiriwa kuua watu 40,000. Hili linadhihirisha wazi kuwa binadamu ameshindwa na hatoweza kamwe kuleta amani ya kudumu ulimwenguni, katika muktadha huo tunalazimika kukubaliana na nabii Yeremia aliyeongozwa na roho takatifu kuandika kuwa "njia ya mwanadamu haimo katika uwezo wake, Mwanadamu anayetembea hana uwezo wa kuongoza hatua yake."
Pamoja na jitihada nyingi zilizofanywa na wanadamu kwa kipindi kirefu ili kurejesha amani ya ulimwengu, bado juhudi hizo zimeishia patupu kutokana na ushawishi mkubwa anaoufanya mtawala wa dunia hii. Katika kitabu cha Ufunuo 12:7-9 Biblia takatifu inatuambia kuwa "Na vita vikatokea ghafla mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, naye joka na malaika zake wakapigana nao. Lakini hawakushinda, wala mahali hapakupatikana tena mbinguni kwa ajili yao. Basi yule joka mkubwa akatupwa chini, yule nyoka wa zamani, anayeitwa Ibilisi na Shetani, anayeipotosha dunia nzima inayokaliwa; akatupwa chini duniani, na malaika zake wakatupwa chini pamoja naye" Habari hii inaonyesha kuwa ibilisi ndiye alikuwa chanzo cha vita hiyo kubwa iliyotokea kule mbinguni, lakini habari njema ni kuwa hakufua dafu dhidi ya jeshi imara la Mwenyezi Mungu lililoongozwa na malaika Mikaeli. Basi Mungu akaamuru fedhuli huyo atupwe chini duniani ili wanadamu wajithibitishie jinsi kiumbe huyo alivyo mwovu, ili hukumu yake itakapotekelezwa iwe ya haki na asipatikane mtetezi yeyote dhidi yake. Lakini kwenye kitabu hicho cha Ufunuo 12:12 malaika wa Mungu anatoa onyo kwa ulimwengu huu akisema "Ole wa dunia na wa bahari, kwa sababu Ibilisi ameshuka kwenu, akiwa na hasira kali, akijua kwamba ana kipindi kifupi cha wakati.” (Soma pia 1Yohana 5:19) Tangu kiumbe huyo mwovu alipotupwa duniani amekuwa akiwachochea wanadamu kuwafanyia ukatili wengine. Amesababisha amani ya ulimwengu huu kupotea. Nia yake ni ile ile aliyoionyesha kule mbinguni, hataki amani.
Lakini hii haimaanishi kuwa hatuwezi kamwe kupata amani na kufurahia maisha. Lipo tumaini zuri ajabu ambalo Mwenyezi Mungu amewaahidi wanadamu wote waadilifu dhidi ya manyanyaso yanayotokana na vita. Katika kitabu cha Nabii Isaya 2:4 Maandiko yanasema "Atatekeleza hukumu miongoni mwa mataifa, Na kunyoosha mambo kuhusiana na watu wengi. Watafua panga zao ziwe majembe ya plau, Na mikuki yao iwe miundu. Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa lingine,Wala hawatajifunza vita tena kamwe."
Ili kupata amani na furaha katika kila nyanja maishani mwetu hatuna budi kuimarisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu aliyechanzo cha amani. Kwa kadri utakavyozidi kujifunza neno la Mungu na kulielewa ndivyo jinsi utakavyozidi kupata amani itokanayo na kuijua kweli. Huenda maisha yanakulemea, ndoa yako ina matatizo au shida yoyote ile, muombe Mwenyezi Mungu huku ukitia bidii kusoma neno lake naye atajibu. Kwani imeandikwa "Mwenye furaha ni mtu ambaye hatembei katika mashauri ya waovu, Na hasimami katika njia ya watenda dhambi, Naye haketi katika kiti cha wenye dhihaka. Lakini anapendezwa na sheria ya Yehova, Naye huisoma sheria Yake kwa sauti ya chini mchana na usiku" Zaburi 1:1-2.
Endeleeni kuwa imara mkidumu katika Upendo wa Mungu na Kristo wetu.
Amina!



Maoni
Chapisha Maoni